UWEKEZAJI BORA KWA MAZAO BORA YA MITI
Uwekezaji Bora.
Uwekezaji wa kupanda miti unachukua muda mrefu kidogo
ukilinganisha na mazao mengine ya nafaka hivyo toka muda wa kupanda inaweza
kuchukua si chini ya miaka minne kwa Mikaratusi/Milingoti/Eucalyptus na miaka
nane hadi kumi kwa Mipaina/Pines ndiyo uanze kuvuna. Unatakiwa kwenda nayo
taratibu hivyo kila mwaka unaweza kupanda miti kiasi/heka chache ili
utakapoanza uvunaji uendelee kuvuna kila mwaka na kupanda tena ulikovuna.
NB: Lakini pia hili linategemea na malengo binafsi au kulingana na
kipato cha uwekezaji.
Kuhusu gharama za kununua na kupanda Miti zinatofautiana kufuatana
na sehemu/mahali husika. Lakini kichocheo kikubwa huwa ni miundombinu na hali
ya hewa nzuri kwa ustawi wa Miti. Kwa wakati huu maeneo mengi yenye rutuba na
miundombinu nzuri yamepata wateja wengi na kupelekea wamiliki kupandisha bei ya
Ardhi katika miaka ya hivi karibuni. Bei ya hekali moja kwa sasa inaanzia TSh
70,000/= kwa maeneo yaliyo mbali zaidi lakini inafika hadi 300,000/= kwa maeneo
yaliyo na miundombunu nzuri na ambayo yapo karibu na barabara kuu. Pia bei ya shamba inaweza kupungua kulingana
na ununuaji wa shamba lenye hekali nyingi zaidi. Vilevile bei ya miche ya Miti
pia inapishana kutoka sehemu moja hadi nyingine ila kwa maeneo mengi mche wa
mti wa Mpaina/Mlingoti huuzwa kwa bei ya wastani wa TSh. 150/=.
Mazao Bora ya
Miti:
Kiasi cha mazao ya miti kama mbao, nguzo, kuni na mirunda/mijengo
utakazopata zitagemeana na vitu vifuatavyo;
ü Ubora wa shamba
na Aina ya miti ya Kupanda,
ü Utumiaji wa Mbegu
bora,
ü Uandaaji wa
shamba na Nafasi ya Upandaji Miti(spacing),
ü Matunzo ya Miti,
ü Umri wa Miti na
Namna ya Uvunaji.
Ubora wa Shamba
na Aina ya Miti Kupanda.
Rutuba na udongo wenye uwezo wa kupitisha maji kiasi na
kuyahifadhi kwa muda mrefu ni sifa kubwa katika ustawi wa miti. Kwani miti inahitaji
maji na virutubisho kutoka katika ardhi hivyo uwezo wa udongo kwenye shamba ni
muhimu kuzingatiwa. Maeneo mengi ya nyanda za juu kusuni yana bahati ya kuwa na
mvua nyingi na hali ya hewa inayowezesha miti hii ya kigeni kuweza kustawi na
kukua kwa haraka. Wastani wa mvua kwa mwaka ni muhimu kuzingatiwa kulinga na
aina ya miti inayotakiwa kupandwa.
Nashauri hili kwa sababu kwa wakati huu kuna wadau wengi
wamejitokeza kujihusisha na udalali wa ardhi lakini pia madalali hao
huwashawishi wawekezaji/wateja wao kuandaa na kuwapandia Miti katika mashamba
yao. Hii hupelekea wengi wao kuweza kutumia njia rahisi na mbegu za bei ya
chini ili kutaka kupata faida zaidi. Hii ni mbaya zaidi kwa wakulima
wageni/wanaoanza uwekezaji huu kwani madhara yake huanza kuonekana baada ya
mwaka wa pili na tatu ambapo hupelekea mkulima kupata hasara kubwa. Hasara hii
husababishwa na Miti kufa na kudhoofika na kupelekea kutoa mazao duni. Pia
ubora wa shamba uendane na ghalama kwa kuzingatia vitu muhimu kama rutuba,
upatikanaji wa mvua, mteremko wa wastani na miundombinu nzuri ya barabara. Nashauri
usikubali kukodishiwa shamba kwa ajili ya upandaji miti kwani huu ni uwekezaji
wa muda mrefu na ardhi ni sehemu ya uwekezaji pia. Sehemu ambayo upandaji wa
miti umeshika kasi sana lazima ardhi itakuwa aghali kidogo japokuwa ndiyo
sehemu nzuri kwani wananchi wake watakuwa na uzoefu wa upandaji miti na hutakuwa
peke yako itakuwezesha kupata nguvu kazi pamoja na kudhibiti moto kirahisi.
Miti ya mipaina na milingoti/mikaratusi huhitaji rutuba na mvua za
kutosha katika kuimarisha ustawi mzuri lakini baadhi ya miti ya
milingoti/mikaratusi inauwezo wa kustahimili kwenye maeneo yenye mvua za
wastani. Maeneo yenye miteremko sio mazuri kwa kilimo cha milingoti/mikaratusi
kwani miti hii huhitaji kufanyiwa usafi/palizi vizuri hasa mwaka wa kwanza na
pia uvunaji wa mazao yake kama mirunda na nguzo huwa rahisi kusafirishwa kwa
lori kufika shambani.
Utumiaji wa Mbegu
Bora.
Utumiaji wa mbegu bora za Miti huwezesha miti kukua kwa haraka na
pia Miti kuwa na ubora unaofanana. Hii
ni muhimu kwani Miti inayokuwa kwa haraka ina uwezekano wa kupona kwa asilimia
kubwa (survival) baada ya kupandwa.
Mfano: Heka moja inayoweza
kuchukua Miti 450 hadi 620 inaweza kuwa na survival ya 80% ya miti hiyo baada
ya mwaka wa kwanza wakati shamba la Mbegu za kawaida inaweza isifikie hata 50%
ya miti yake shambani. Kufanana kwa miti ni huku kama miti imepandwa mwaka
mmoja na mbegu moja iliyoboreshwa mara nyingi hustawi kwa kimo na ubora
unaofanana.
Mbegu bora za miti ni zipi?
Kwa kifupi mbegu nyingi za mipaina na Milingoti tunazozipanda
zimemezalishwa kutoka kwenye miti ambayo iliingizwa na wazungu wakiwemo
wakoloni na wamisionari kwenye miaka ya 1930’s ambazo walizipanda kwenye mikoa
ya Iringa, Mbeya, Arusha na Kilimanjaro ambako walianzisha mashamba. Hivyo
kutoka miaka hiyo hadi sasa unaweza kuona kuwa na miti ya uzao wa nne ambayo
imekuwa kwa mzunguko(rotation) wa miaka 20. Kumbuka tangu mbegu hizi kuingia nchini
hakuja wahi kuwa na mashamba maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za
Miti hapa nchini hata nchi za Afrika Mashariki.
Mbegu bora za miti huzalishwa kwenye shamba maalum liitwalo kwa
kimombo Seed Orchard. Maandalizi ya
shamba hili kwanza kabisa huanzia kwenye mbegu na hapa huchaguliwa miti maalumu
kwa mazao maaluum.
Mbegu wa ajili ya miti ya mbao huchaguliwa kutoka kwenye uzao wa
miti iliyo na sifa ya kukua kwa haraka na kwa kunyooka ili kupata mbao zenye
ubora na kwa muda mfupi. Vilevile mbegu kwa matumizi ya kuni huchaguliwa kutoka
katika uzao wa miti inayotoa nishati nzuri ya moto na pia inayokua kwa haraka.
Mbegu hizi huchambuliwa mbegu zenye uwezo wa kuota vizuri na
kuhakikisha mama zao hawana matatizo mengine kama magonjwa baadaye kupandwa
kwenye mashamba maalumu ambayo hutengwa na mashamba ya kawaida ili kuepuka
kuchanganya mbegu wakati wa uchavushaji. Baada ya miaka isiyopungua 20 zoezi
hili hurudiwa kwa kuchukua mbegu mpya za uzao huu na kupandwa tena ila katika
awamu hii uangalizi na udhibiti wa uchaushaji huboreshwa zaidi na kuhakikisha
tukio hilo linasimamiwa na ikiwezekana hufanywa na binadamu badala ya wadudu
kama nyuki na vipepeo. Baada ya miaka 20 tena ndio sasa mbegu huvunwa na
kuchambuliwa mbegu zenye ubora wa kuota vizuri na ndio tunaweza kuziita MBEGU
BORA. Kwa sasa mbegu bora zinazalishwa zaidi nchi za Afrika ya kusini, Zibwabwe
kwa Afrika.
NB: Kuna mbegu zinaitwa Clone
seeds hizi hutokana na kukopi genes za uzao mmoja na kuuunganisha na uzao
mwingine wa mti kwa jamii ile ile au tofauti na ile. Zoezi hili huanzia maabara
na baadaye kuendelea shambani. Huku shambani baada ya mbegu iliyopatikana
kuzalishwa huoteshwa na baada ya kukua kwa muda kama mwaka mmoja, mti huu
kukatwa ili kusababisha machipukizi ambayo hutolewa vikonyo na kuchomekwa
kwenye viriba au majaruba ili kuzalisha miche ya miti. Miti hii hupewa majina
kutokana na uzao wake, Mfano: GC514 hapa G inawakilisha uzao wa Eucalyptus
grandis na C ni Eucalyptus camaldulensis hapo hii Na; 514 inakuwa kama namba ya
usajili au utambuzi kwani hubeba maelezo zaidi ya namna hatua za maabara
zilivyofanyika. Kumbuka miche ya Clone
seeds huzalishwa kutoka kwenye vikonyo vya mti mmoja na sio kwa kutumia
mbegu, hii huipa sifa miti ya clone
kuwa na sifa zinazofanana zaidi kuliko miti iliyopandwa kutokana na mbegu.
Uandaaji wa
shamba na Nafasi ya Upandaji Miti (spacing)
Uandaaji
wa shamba ni vizuri liandaliwe kwa kulilima lote kwa kutumia jembe la mkono,
trekta au jembe la kukokotwa na ng’ombe ndio kunapendekezwa zaidi. Pia unaweza
lima upana wa mita moja katika mstari wa kupanda miti au kulima visahani vya
upana wa mita moja na sehemu iliyobaki kufyeka majani yote. Aina hizi tatu ndio
zinazoshauriwa zaidi kwa ukuaji wa haraka na kupata mazao bora zaidi.
Nafasi
kutoka mti hadi mti unashauriwa uwe ni mita 3x3 hasa kwa miti ya mipaina ili
kuweza kutanuka zaidi. Nafasi hii huwezesha miti kuweza kupata mwanga na
chakula cha kutosha tangu kupandwa hadi inapofikisha umri wa miaka mine. Kwa
miti ya milingoti/mikaratusi ambayo hasa inayopandwa kwa mazao ya mirunda
inaweza kupandwa nafasi ya mita 2.5x2.5 kwani miti hii huhitaji kurefuka zaidi kuliko
kutanuka.
Matunzo ya Miti.
Baada
ya kupanda miti kwenye shamba utunzaji wa miti ni muhimu ili kuimarisha ustawi
wa miti hiyo. Kama nilivyo dokeza mwanzoni miti ya milingoti/mikaratusi
inahitaji usafi zaidi kuliko mipaina. Hivyo hakikisha shamba lako la miti
linapaliliawa lota kama shamba la mahindi
kwani hii ndio njia bora ya ukuaji haraka na unaozuia majanga ya moto na
magonjwa ya miti kwa kiasi cha juu. Njia nyingine ni kupalilia visahani au
kufyeka majani yote shambani njia hii inafaa hasa kwa miti ya mipaina. Palizi
mara nyingi huwa ni kwa miaka miwili hadi mitatu pale miti itakapoanza kufunga
baada ya matawi yake kukua.
Kupogolea
(Pruning) ni muhimu sana kwa miti ya mipaina kwani miti ya milingoti haihitaji
kupogolewa kwa sababu huwa inajipogolesha yenyewe (self-pruning), ugoleaji
uanze kuanzia mwaka wa tatu toka miti kupandwa kwa kuzingatia ukuaji wa matawi
ya chini kutoka mti hadi mti kukua kiasi cha kugusana na ufanyike kwa kutumia
kisu au panga lenye makali kwa kukata tawi karibu kabisa na shina la mti. Tukio
hili lifanyike kipindi cha kiangazi wakati mvua zimesimama ili kuharakisha
uponaji wa kidonda/kovu na kupunguza miti kuoza.
Kupunguzia
miti (thinning) ni moja ya hatua muhimu kwenye utunzanji wa shamba la miti na
ambayo wakulima wengi hawaizingatii. Kupunguzia miti ni kuondoa baadhi ya miti
shambani ili kuipatia miti iliyobaki nafasi zaidi kwa upatikanaji wa mwanga wa
jua na maji ardhini. Lakini hili pia huzingatiwa kutokana na aina ya mazao
yanayotarajiwa. Kitaalamu tunashauri ili kupata mbao pana zaidi na nguzo kubwa
za umeme mkulima lazima aache nusu ya miti shambani ifikapo mwaka wa kumi. Kwa miti iliyopandwa kwa ajili ya mazao
ya kuni na karatasi sio lazima kupunguziwa.
Njia
za kuzuia moto (Fire Lines) zinatakiwa zitengeneze kila mwaka baada tu ya msimu
wa mvua kuisha bila kukosa kuzingatia ukubwa wa shamba lako. Ni vizuri na
rahisi kuweka njia ya moto kwenye shamba kubwa kuanzia heka kumi ili kupunguza
ghalama na upotevu wa eneo la uzalishaji. Angalau uweke njia ya moto yenye
upana wa mita tano hadi kumi kutoka shamba moja hadi jingine kwani njia hizi
pia zitatumika wakati wa uvunaji kwa ajili ya kupitisha magari.
Pia
ulinzi wa magonjwa mbalimbali lazima uwepo ili kuhakikisha miti yenye tatizo
inatibiwa au kukatwa na kuchomwa ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa shambani.
Ila kwa sasa tunabahati ya kutokuwa na magonjwa mengi nchini mwetu hivyo hili
sio la kuhofiwa sana.
Umri wa mti na
namna ya uvunaji.
Kama mambo manne hapo juu yakizingatiwa basi thamani na ubora wa
mazao ya miti yatategemea umri wa mti shambani. Mara nyingi umri wa mti ndio
unaoelekeza bei katika kilimo cha miti hivyo thamani ya shamba la miti
huongezeka thamani kutoka mwaka hadi mwaka.
Mfano; maeneo
mengi ya mkoa wa Njombe shamba lenye miti ya mipaina au milingoti/mikaratusi
yenye umli wa mwaka mmoja linauzwa kuanzia TSh. 1,000,000/= hadi 2,000,000/=.
Wengi wetu miti ya mipaina ikifika umli wa miaka 12 tunavuna, na
kinachopatikana siyo haba lakini nadhani ni vizuri zaidi kuvuna kuanzia miaka
15 au 20 hivi kwani utakuwa na uhakika wa kupata pingili ndefu siyo chini ya
mbili zenye urefu wa futi 12 na mbao za 2x6 angalau 6 na kwenda juu Kwa kawaida tegemea
kupata kati ya mbao tano za 2x6 kama ukiharakisha kuvuna lakini mti huo kama
umekomaa (miaka 20 hivi) umetunzwa vizuri na ulipandwa kwa nafasi nzuri unaweza
kutoa hadi mbao 10. Ubao mmoja wa 2x6 uliowekwa dawa (treated timber) katika
jiji la Dar es salaam unauzwa siyo chini ya TShs 17,000/= na ukiwa bado Njombe
kiwandani bila dawa ni Shs 10,000/=. Kwa miti ya milingoti/mikaratusi inaweza
kuvunwa baada ya miaka minne kwa zao la mirunda ambayo huuzwa kuanzia TShs.
3000/= kwa mti na baada ya miaka sita miti hii huweza kutoa mazao ya nguzo
ndogo za fensi na umeme yenye thamani ya TShs. 10,000/=. Baada ya kupunguzwa
shambani miti hii hutoa zao la nguzo kubwa za umeme, mbao pamoja na kuni ambapo
kila mti unathamani ya TShs 50,000/=.
Uvunaji wa kisasa ni ule unaozingatia ubora wa mazao ya miti hasa
umli pia kuhakikisha uvunaji unafanyika kwa vifaa bora kama chain saw kuangusha
na kuakata matawi na table saw kwa ajili ya kuchana mbao.
safi sana
ReplyDeleteAsante.
DeleteWaheshimiwa,
ReplyDeletenatarajia kuanzisha mradi wa misitu ukilenga "carbon offsetting". Ningependa kuja ni miti ya haina gani inaweza kutumiwa. Kama wenye blog hii bado mko hewani naomba mniandikie E-Mail (hannes.kreissl@gif-ev.org)
Sawa nitakuandikia email.
DeleteAsante.
Nimevutiwa na kilimo cha miti Nina eneo kubwa maeneo ya mkata naomba ushaur wa kitaalam niweze kupanda miti katika eneo hiloo
ReplyDeleteHlw team, nimefurahia mada yenu.
ReplyDeleteNaomba mnipatie contacts zenu kwa email mwailengeism1919@gmail.com.
Asanteni