USIYOYAJUA HUHUSU KILIMO CHA MITI

Tree Farmers from Sapanda village in Ileje sells the unpotted Pines seedlings in Isangati village in Mbeya rural, Feb2015.
Kilimo cha miti kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya mazingira. Katika Tanzania, Mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa maarufu inayoongoza kwa misitu mikubwa ya kupandwa. Miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea nyumba na utengenezeaji wa karatasi.

Ukiacha mahitaji haya tuliyoyazoea hivi sasa kumeibuka fursa nyingine mpya ambako mashirika ya kimazingira kutoka Magharibi yananunua hewa ukaa (carbon dioxide). Kwa maana hiyo unaweza kupanda shamba la miti halafu ukawa unakusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae uvune mbao, nguzo au miti ghafi ya kutengenezea karatasi.

Binafsi niliichangamkia biashara hii miaka minne iliyopita na 'I'm real serious with it'. Nimejiwekea lengo la kupanda ekari 20 kila mwaka. Kilimo hiki cha miti ni uwekezaji wa muda wa kati na mrefu (middle & long term investments). Kiutamaduni Watanzania wengi huwa hawavutiwi na uwekezaji wa muda mrefu.

Hata hivyo, kama una mpango wa kuwa na baadaye imara kiuchumi usikwepe kufikiria uwekezaji wa muda mrefu. Waingereza husema "Information is power". Wengi hawajachangamkia fursa hii kwa kukosa taarifa tu. Kazi yangu leo ni kukupa taarifa hizi za utajirisho.

Ekari moja ya shamba inachukua wastani wa miti 600. Wastani wa chini wa mti mmoja kwa sasa uliokomaa ni Sh 20,000. Ina maana katika ekari moja ukiwa na miti iliyokomaa unakusanya Sh milioni 12. Fedha hiyo (kadirio la chini kabisa) utaipata ikiwa unaamua kuuza kwa bei ya jumla miti ikiwa shambani. Lakini kama ukiamua kupasua mbao wewe mwenyewe unaweza kuvuna mbao hadi za 25,000,000 kwa ekari moja.

Gharama ya kununua shamba tupu ni kati ya Sh 200,000 hadi Sh milioni moja kutegemea na maeneo husika unayotaka au kupata. Gharama za kuandaa shamba, kununua miche na kupanda ni kati ya Sh 400,000 hadi Sh 600,000. Hii ina maana unaweza kumiliki ekari moja ya msitu wa miti kwa hadi Sh 600,000 tu.

Kilimo cha miti ni rahisi sana kwa sababu ukishapanda hakihitaji uangalizi mkubwa sana na wala hauhitajiki uwe karibu na shamba/mradi muda wote. Kuna kazi chache ambazo zinahitajika ukishapanda shamba lako. Mvua inyeshe au isinyeshe mti wa mbao, nguzo au karatasi ukishachipua huwa haufi kwani huendelea kutumia unyevu wa ardhini.

Kazi namba moja unapokuwa umeshakamilisha upandaji wa miti kwenye shamba, ni kutengeneza njia za kuzuia moto walau mara moja kwa mwaka. Kazi ya pili ni kufyekea miti inapokua walau kwa mwaka mara moja. Gharama zote hizo, yaani kutengeneza njia za moto, kufyekea na kulinda moto haizidi Sh 200,000 kwa mwaka mzima.

Miti hukomaa kuanzia miaka sita hadi 10 kutegemea na utunzaji unaoufanya. Hii ina maana kuwa ukichukua Sh 200,000 unazogharimia shamba kila mwaka ukazidisha mara sita unapata Sh 1,200,000.

Kwa maana hii gharama za kuhudumia shamba la miti ekari moja kutoka kupandwa hadi kuvunwa ni kati ya Sh milioni 1.2 hadi Sh milioni mbili. Ukichanganya na gharama ya kupata ardhi na kupanda miti yenyewe unapata kuwa gharama nzima hadi unavuna ni kati ya Sh 2,000,000 kwa kadirio la chini.

Hapa ili kuokoa nafasi nimeweka makadirio yaliyochanganya milinganyo ya muda wa kuvuna, eneo unalopata pamoja na thamani ya fedha katika muda husika. Gharama hizi ninazopiga ni ikiwa utaamua kununua shamba leo na kama ungekuwa tayari una shamba ambalo unalihudumia leo.

Hata hivyo, nadhani wote tunafahamu kuwa ardhi ni rasilimali inayopanda thamani kila siku. Vile vile tunatambua kuwa suala la mazingira ni tete kwa sasa na katika karne zijazo kama wataalamu wanavyotuthibitishia. Hii ina maana kuwa ukiwa na shamba la miti leo, thamani ya ardhi hiyo inazidi kupanda kila siku na miti uliyopanda inazidi kupanda thamani kila kukicha.

Jambo la uhakika ni kuwa hata kama bei ya miti, mbao, nguzo itayumba hutaweza kupoteza mtaji uliotumia na wala hutakosa kuzalisha faida kwa shamba utakalokuwa umemiliki, iwe ni eka moja, kumi, mia au elfu moja. Mbali na hivyo unaweza ukaona, ahaa, miaka sita hadi 10 ni mingi mno; bado una nafasi ya kupata faida hata ndani ya mwaka mmoja, miwili na kadhalika.

Ukishapanda shamba la miti ekari moja kisha baada ya mwaka mmoja ukaamua uuze utauza si chini ya milioni mbili hadi nne. Kukusanya milioni nne kwa mtaji wa laki sita, pasipo kutumia muda mrefu au usumbufu wa kusimamia, hakika ni faida nono.

Huenda hadi kufika hapa unaweza ukawa umeshavutiwa na biashara hii. Wengi wenu mnaweza kujiuliza maswali makubwa mawili; "Ninatamani nifanye mradi huu, lakini Iringa sikufahamu na hata kama nakufahamu nitaanzia wapi kupata hayo maeneo?" Pili, "Niko mbali na sina muda wa kushinda Iringa, je, ni nani atanisaidia kupanda, kusimamia na kuendesha hayo mashamba?"

Kama si hayo maswali mawili hapo juu huenda ningekuwa nilishaandika makala hii tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Lakini nilisita kuandika fursa hii mapema pasipo kuwa na majibu ya maswali hayo kwa wasomaji. Leo nina majibu hayo. Pia nikujulishe kuwa msimu wa kutafuta na kuandaa mashamba tunaanza Agosti-Oktoba na upandaji ni Novemba-Desemba hadi Januari kwa wanaokuwa wamechelewa.

Sifa kubwa ya ujasiriamali ni kufanya huduma kwa watu wengine, yaani kutafuta mahitaji, shida, matatizo na matamanio yao na kuwatimizia. Kama alivyosema mfanyabiashara mmoja wa Kimarekani, Zig Ziglar; "Utapata unachokitaka ikiwa utawasaidia watu wengine wengi kupata wanachokitaka".

Katika kuwasaidia wengine ili wawekeze katika biashara hii ya mashamba ya miti ninaongozwa na mambo makubwa mawili ninayotaka kuona yakitimia. Mosi, mimi na wewe tuungane na serikali na dunia nzima katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupanda miti mingi.

Pili, nataka nikusaidie wewe ambaye kila siku nimekuhamasisha ufikirie biashara na uwekezaji, uchukue hatua ya kuwekeza ili ujikwamue kiuchumi kwa kuvuna mamilioni. Moja ya ndoto nilizonazo duniani ni kuzalisha na kuendeleza wafanyabiashara na wawekezaji wapya kwa maelfu hadi naingia kaburini. Huo ndiyo wito wangu duniani.

Ili kutimiza ndoto yangu hiyo, nimeweka utaratibu ufuatao utakaohakikisha kila mwenye ndoto, kiu na hamasiko la kuwekeza kwenye kilimo cha miti anafanikiwa. Kupitia mfumo wa biashara zangu nimeanzisha kitengo maalumu kijulikanacho kama Fresh Farms (T).

Kazi yangu kupitia kitengo hiki itakuwa ni kukupa ushauri wa kibiashara, kukutafutia maeneo ndani ya Mkoa wa Iringa kwa ekari unazotaka, kukuandalia hayo mashamba, kukupandia hiyo miti na kusimamia utunzaji wa shamba katika hatua za awali na hata baadaye. Jisikie huru wakati wowote kuwasiliana nami kwa ufafanuzi na msaada wa fursa hii.

Kwa kutumia sheria, taratibu na tamaduni zote za wenyeji zinazohusiana na umilikaji ardhi nitahakikisha nakusaidia ili ndoto yako itimie. Nadhani kwa utaratibu huu ipo siku nami naweza kusimama na kujivunia mazao ya watu waliokombolewa kivitendo kutokana na harakati zangu za kuelimisha watu kuhusu ujasiriamali, uchumi na biashara.

Comments

  1. Kwa namna gani tunaweza kuwasiliana

    ReplyDelete
  2. Unapatikanaje ndugu?
    Please write me in my email address "fabriceruba@gmail.com"

    ReplyDelete
    Replies
    1. Karibu sana, nimekutumia email. au nipigie 0758116818.

      Delete

Post a Comment

Popular posts from this blog

THAMANI YA SHAMBA LA MIPAINA/PINES HAIPO KWENYE WINGI WA MITI

UWEKEZAJI BORA KWA MAZAO BORA YA MITI